Upo uwezekano kwa klabu ya Manchester United kurudia nia yake ya
kutaka kumsajili winga machachari, kipaji halisi cha soka kutoka nchini
Colombia anakipiga FC Porto ya Ureno James Rodriguez. Inavyoonekana Man
United inaweza ikafanikiwa kupata huduma ya mchezaji huyu endapo tu
itakubali kubadilishana moja ya wachezaji wao ghali...anaweza akawa
Anderson au Antonio Valencia.
Rodriguez mwenye miaka 21 tu hivi
sasa, amekuwa kwenye mawindo ya Sir Alex Ferguson kwa mda mrefu sasa
tangu kipindi cha dirisha kubwa la usajili barani Ulaya katikati ya
mwaka uliopita wa 2012. Man United ilipeleka ofa FC Porto lakini kwa
bahati mbaya ilikataliwa. FC Porto walihitaji £36m, pesa ambayo ilikuwa
ngumu kidogo United kukubali kuitoa.
Hata hivyo, kumekuwa na
taarifa kutoka vyanzo mbalimbali nchini Uingereza kuwa kiungo Anderson
angependa kurudi kwenye klabu yake ya zamani (FC Porto) kitu ambacho
binafsi ninahisi kitasaidia kufanikisha lengo la United kumnasa
Rodriguez.
Anderson amejikuta akiwa kwenye wakati mgumu ndani ya
Manchester United kutokana na kushindwa kurudia fomu yake tangu apatwe
na tatizo la kuandamwa na majeruhi na amekuwa akikabiliwa na upinzani wa
hali ya juu kupata nafasi kwenye kikosi cha kwanza kutoka kwa kina
Michael Carrick na kinda Tom Cleverley jambo ambalo linachochea hamu
yake ya kutafuta timu nyingine atakayoichezea michezo mingi ili mwisho
wa siku aitwe kwenye kikosi cha timu yake ya taifa ya Brazil
kitakachocheza fainali za kombe la Dunia mwakani.
Pia kwa mujibu
wa taarifa mbalimbali, ni wazi kwamba Manchester United inataka
kuondokana na mchezaji huyo ambae kimsingi mtu anaweza kumuita 'injury
prone player' yani mchezaji anaesumbuliwa na majeruhi ya mara kwa mara.
United inataka kumrejesha Anderson FC Porto ili kuwe na urahisi fulani
wa kumpata Rodriguez.
Na jambo lingine la kufurahisha ni kwamba
msaka vipaji wa Man Utd Martin Ferguson ameki-scout kipaji hiki mara 7
msimu huu. Inaonekana sasa ni wazi kwamba Sir Alex Ferguson atawapa FC
Porto Anderson na atatuma ofa mpya ya kutaka kumnasa Rodriguez.
James
Rodriguez ameanza michezo 11 msimu huu na amefunga mabao 8 kwenye ligi
kuu ya Ureno, na kama atajiunga na wababe hao wa soka la Uingereza
itamaanisha atakuwa amejiunga na washambuliaji wa kiwango cha Dunia
(World Class Players) Wayne Rooney na Robin van Persie kwenye safu ya
ushambuliaji ya Manchester United...Rodriguez anasemwa kuwa bidhaa
muhimu sana ambayo soka la Ulaya na Dunia kwa ujumla inajivunia nae.
Safari
hii, mawinga wa United hawajaonesha makali sana tofauti na misimu
kadhaa iliyopita. Baadhi yao wameporomoka viwango hasa Antonio Valencia
ambae msimu uliopita ndie alikuwa mchezaji bora wa mwaka wa Manchester
United...Ikiwa tayari Man United wameshamnasa Wilfried Zaha katika
dirisha dogo la usajili lililopita la mwezi januari, ni wakati sasa wa
United kuanza kutumia damu mpya kwenye 'flanks' ili kurejesha zile
'glorious days' kama za enzi ya Cristiano Ronaldo.
Zaidi ya hayo,
James Rodriguez amekuwa akitajwa kama ndie Cristiano Ronaldo wa Amerika
ya kusini kutokana na uwezo wake mkubwa alionao wa kusakata kabumbu. Pia
mwenyewe alifarijika sana pindi aliposikia taarifa za kutakiwa na
Manchester United msimu uliopita na baadae kunukuliwa akisema siku moja
angependa kuchezea moja ya vilabu vikubwa barani Ulaya na akazitaja timu
za Manchester United, Real Madrid na FC Barcelona.
Kwa kumalizia,
kama Man United itafanikiwa kumsajili Rodriguez basi bila shaka itakuwa
na safu moja kali sana ya ushambuliaji na haitakuwa ikipigania Ubingwa
wa EPL pekee bali pia Ubingwa wa FA na Ubingwa wa Ulaya yani ile UEFA
Champions League...TUSUBIRI TUONE!